Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amekabidhi mitungi ya gesi kwa wananchi wa Kijiji cha Kilangala, Jimbo la Mchinga mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Makamu wa Rais amekabidhi mitungi hiyo leo Novemba 15, 2026, alipotembelea mradi wa nishati safi ya kupikia katika kijiji hicho akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Lindi.
Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kulinda afya za wananchi, hususan wanawake, kuhifadhi mazingira na kupunguza gharama za maisha.
Serikali imeweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mitungi hiyo, Mhe. Ndejembi amempongeza Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Kikwete, kwa kuwasemea wananchi na kusimamia mahitaji yao ya maendeleo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutekeleza miradi ya maji, umeme, barabara, afya na uvuvi ili kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi wa jimbo hilo.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Lindi, baada ya kutembelea mikoa ya Ruvuma na Mtwara katika mwendelezo wa ziara zake za kikazi nchini.















إرسال تعليق