VIJANA 985 WANAOKWENDA KUFANYA KAZI NJE YA NCHI WAAGWA



Na. OWM (KAM) – Dar es Salaam


Serikali imeonya kuwa haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawakala binafsi wa huduma za ajira au mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na udanganyifu, ukiukwaji wa taratibu za ajira au usafirishaji haramu wa Watanzania kwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa Novemba 2026, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus C. Sangu, wakati wa hafla ya kuwaaga vijana 985 wanaokwenda kufanya kazi katika nchi mbalimbali nje ya Tanzania.

Mhe. Sangu alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mawakala binafsi wa huduma za ajira katika kuwaunganisha Watanzania na fursa za ajira ndani na nje ya nchi, lakini akasisitiza kuwa mchango huo unapaswa kuendana na uzingatiaji wa sheria, weledi, uwazi na uwajibikaji.

Akizungumza na vijana hao, Mhe. Sangu alisema Serikali ina imani nao na kuwataka kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi, huku wakizingatia sheria, mila na desturi za nchi wanazokwenda kufanya kazi.

“Tumieni ujuzi wenu kujenga imani kwa waajiri na kufungua fursa zaidi kwa Watanzania wengine. Kila mmoja anatakiwa kuwa tayari kujituma na kutumia fursa hizi kama chachu ya kuboresha maisha yake, kuinua familia yake na kuchangia maendeleo ya Taifa,” alisisitiza Mhe. Sangu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu alisema Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia majukwaa mbalimbali yanayolenga kuratibu uhamaji salama wa nguvukazi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

Aidha, aliwahimiza vijana kuendelea kuomba nafasi za ajira za mafundi zilizotangazwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), akitangaza kuongeza muda wa kuwasilisha maombi hayo kutoka Novemba 3 hadi Novemba 8, 2026, ili kuwapa nafasi waombaji wengi zaidi kushiriki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima, aliwataka vijana hao kufanya kazi kwa bidii, kutunza nyaraka zao muhimu na kutumia njia rasmi za mawasiliano wanapohitaji msaada.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Neema Moshi, alisema Ofisi hiyo itaendelea kuratibu upatikanaji wa fursa za ajira kwa vijana kwa lengo la kuchochea ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Robert Kadege, ambaye ni Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Mfuko huo, aliwapongeza vijana hao kwa kujiunga kwa wingi katika mfumo wa hifadhi ya jamii ili kujiwekea akiba na kuimarisha usalama wao wa kifedha wa baadaye.

Akizungumza kwa niaba ya mawakala binafsi wa ajira, Mwenyekiti wa mawakala hao, Bw. Abdallah Mohammed, alisema sekta hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kurasimisha ushiriki wa vijana katika soko la ajira la kimataifa.







Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA