SERIKALI YAAHIDI KUFANYA KILA LINALOWEZEKANA WANANCHI WAPATE UMEME

Na. Neema Mbuja,  Mtera

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga ( katikati),  akizungumza jambo mbele ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt. Doto Biteko ( wa kwanza kushoto), wakati wa ziara ya kutembelea Bwawa la kuzalisha Umeme la Mtera, Oktoba 03, 2023.


SERIKALI itaongeza upatikanaji wa gesi ili kufidia mapungufu ya hali ya upatikanaji wa umeme nchini unaochangiwa na upungufu wa maji kwenye mabwawa yanayozalisha umeme.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Mashaka Biteko wakati alipotembelea mradi wa bwawa la kufua umeme la Mtera ili kujionea hali ya maji kwenye bwawa hilo ambalo limeathiriwa na hali ya upungufu wa maji unaosababishwa na ukame kutokana na kuchelewa kwa mvua . 


Mhe. Dkt. Biteko alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na TANESCO itahakikisha inafanya kila linalowezekana kubuni vyanzo vipya ya upatikanaji wa umeme ikiwa ni pamoja na gesi ya kutosha ili kuhakikisha umeme unapatikana ili shughuli za kiuchumi zisiathirike kwa kukosekana kwa umeme. 


"Tahadhari zilizo ndani ya uwezo wetu tunapaswa kuzichukua ikiwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha wananchi wanapata umeme" Alisema Mhe. Dkt Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt. Doto Biteko akiwa kwenye Jumba la Mitambo ya kuzalisha Umeme ( Power house) katika Mradi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Mtera, Oktoba 03, 2023

Alisisitiza kuwa uchumi wa wananchi wa Tanzania unategemea sana upatikanaji wa umeme, hivyo shughuli zozote za kimazingira zikiathiriwa, zinaathiri pia hali ya upatikanaji wa umeme na kuwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji. 


"Serikali inakuja  na mkakati wa pamoja na wadau wa maji na mazingira wakiwemo Tamisemi, Wizara ya maliasili, TANESCO, wananchi na wengineo ili kutunza vyanzo vya maji na mazingira kwani vinategemewa kwenye kuzalisha umeme


Naibu waziri mkuu Mhe.Dkt Doto Biteko alitembelea maeneo mbalimbali ikiwemo jengo la mitambo yaani power house, pamoja na eneo la bwawa la kuzalisha umeme la Mtera.


Pia, ziara hiyo  imehudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga  na Mkurugenzi wa Shirika la umeme Tanzania Mha. Gissima Nyamo Hanga pamoja na Watendaji wengine kutoka shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt. Doto Biteko ( wa kwanza kushoto), akisalimiana na Watendaji kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga  pamoja na Watendaji wengine kutoka shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO),  mara baada ya kuwasili katika Ofisi za  Bwawa la kuzalisha Umeme la Mtera, Oktoba 03, 2023.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt. Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika Ofisi za Mradi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Mtera, Oktoba 03, 2023.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA