TANZANIA YATANGAZA MATOKEO YA UTAFITI WA KITAIFA WA UKATILI DHIDI YA WATOTO NA VIJANA 2024

 


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024, Juni 9,2025 Jijini Dar es salaam - Picha na Kadama Malunde
* Serikali yaahidi kutumia matokeo hayo kupanga mikakati, mipango na programu mbalimbali kupambana na ukatili.

*Yasisitiza Takwimu za Ukatili ni nyenzo muhimu kwa mipango na mikakati ya ulinzi wa watoto na vijana.

*THPS yajivunia kuratibu Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana, yakazia ushirikiano na Serikali kuimarisha ulinzi wa mtoto.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Serikali ya Tanzania imetangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024 (The 2024 Tanzania Violence Against Children and Youth Survey - VACS), ukionesha kupungua kwa viwango vya ukatili wa kingono, kimwili na kihisia kwa watoto wa kike na wa kiume ikilinganishwa na utafiti wa mwaka 2009.

Matokeo hayo yametangazwa leo, Juni 9, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ambaye amesema utafiti huu ni wa pili kufanyika tangu mwaka 2009 na umefanywa kitaalamu kwa ushirikiano wa serikali na wadau wa maendeleo.

"Matokeo ya utafiti huu yanaonesha ukatili umeshuka kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano, kwa watoto wa kike ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 33 hadi 11, kimwili kutoka 76% hadi 24%, na kihisia kutoka 25% hadi 22%. Kwa watoto wa kiume, kingono umepungua kutoka 21% hadi 5%, kimwili kutoka 74% hadi 21%, na kihisia kutoka 31% hadi 16%", amefafanua.
Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024

Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa takwimu hizi zitasaidia serikali kufanya tathmini ya sera, sheria na programu za kisekta kupitia MTAKUWWA II (Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto), ili kuongeza ufanisi wa juhudi za ulinzi wa watoto na vijana.

“Matokeo haya yatawezesha serikali na wadau kuboresha mipango, mikakati na huduma za ulinzi wa watoto kwa kizazi cha sasa na kijacho,” ameongeza Waziri Gwajima.

Athari za ukatili – Hatari za muda mrefu
Waziri Gwajima amesisitiza kuwa ukatili dhidi ya watoto ni ukiukwaji wa haki za binadamu na huleta athari za muda mrefu za kiafya, zikiwemo matatizo ya afya ya akili, mawazo ya kujiua, matumizi ya dawa za kulevya, tabia hatarishi za ngono, maambukizi ya VVU, pamoja na kupungua kwa fursa za kimaendeleo kwa waathirika.
Amesema serikali itaongeza bajeti na rasilimali watu kuimarisha huduma kwa manusura wa ukatili na kuzuia ukatili kwa njia endelevu.

Takwimu ni za Kitaifa na Zinaaminika

Kwa mujibu wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, utafiti huu umefanyika katika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kutumia sampuli wakilishi ya kitaifa, hivyo takwimu zake ni sahihi na zinafaa kutumika kupanga mikakati ya kitaifa.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa

“Huu ni utafiti wa kisayansi wenye viwango vya kimataifa. Takwimu hizi zitatumika kuboresha sera na afua za kitaifa za ulinzi wa mtoto,” amesema Dkt. Msengwa.

Ushiriki wa Wadau wa Kimataifa

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS), Dkt. Redempta Mbatia, amesema kuwa THPS inajivunia kuratibu utafiti huu kwa weledi mkubwa kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (U.S. CDC), na kwa usimamizi mzuri wa Serikali ya Tanzania.
Dkt. Redempta Mbatia akizungumza na waandishi wa habari.

“Utafiti huu umetupatia takwimu muhimu za kusaidia serikali kuongoza juhudi za kitaifa za ulinzi wa watoto na vijana kwa kushirikiana na wadau. THPS tumejidhatiti kuendelea kushirikiana na serikali na wadau katika kutekeleza afua hizi,” amesema Dkt. Redempta.

Ameeleza kuwa matokeo ya utafiti yanaonyesha maendeleo makubwa ya kitaifa katika kupambana na ukatili wa kingono, kimwili na kihisia, na kutoa mwongozo wa kisera na kimkakati kwa serikali na washirika wa maendeleo. 
Bi. Miranda Armstrong akizungumza na waandishi wa habari.

Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka UNICEF, Bi. Miranda Armstrong, amesema shirika hilo limekuwa sehemu ya ufanikishaji wa utafiti huu kama sehemu ya wajibu wao wa kuwalinda watoto.

“Tunaamini kuwa takwimu hizi zitatumika kuimarisha sera, programu na huduma zinazolenga ustawi wa watoto wote nchini,” amesema Armstrong.

Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024 ulilenga kutoa takwimu muhimu za kusaidia serikali kuongoza juhudi za kitaifa za ulinzi wa mtoto. Utafiti uliongozwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (WMJJWMM) Tanzania Bara na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WMJWW) Zanzibar, na kutekelezwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar (OCGS), na kwa msaada wa kitaalamu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Watoto (UNICEF), Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS), na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Serikali ya Marekani (U.S CDC).

Utafiti huu ulifanyika kati ya mwezi Machi na Juni 2024 na uliwahoji watoto na vijana 11,414 wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 24 kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania bara na Zanzibar. Utafiti huu ni wa pili wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto kufanyika nchini Tanzania, utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2009 ambao ulionesha kuwepo kwa ukatili wa kingono,kimwili na kihisia miongoni mwa watoto na vijana.

Ripoti kamili ya utafiti wa ukatili dhidi ya watoto inatarajiwa kutolewa baadaye mwaka 2025. Serikali na washirika wake imejidhatiti kutafsiri takwimu hizi kwa vitendo ikihakikisha watoto na vijana kote Tanzania wanaishi bila ukatili na wafikie huduma za matunzo na usaidizi wanaostahili.

ANGALIA MATUKIO KATIKA PICHA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024, Juni 9,2025 Jijini Dar es salaam - Picha na Kadama Malunde
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa akielezea kuhusu utafiti huo
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa akielezea kuhusu utafiti huo
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa akielezea kuhusu utafiti huo
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA