Meneja wa Barrick nchini, Dk. Melkiory Ngido akimkabidhi mfano wa hundi shilingi billioni Tsh 93.6 kwa mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye hafla ya siku ya gawio iliyofanyika ikulu jijini Dar es Salaam, wengine pichani ni Waziri wa Nchini Ofisi ya Rais (Uwekezaji) Profesa Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Twiga Minerals ,Andrew Mwangakala.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania , Dkt Samia Suluhu Hassan akikabidhi tuzo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Twiga Minerals , Andrew Mwangakala na Meneja wa Barrick nchini, Dk.Melkiory Ngido na wa kwanza kushoto ni Waziri wa Nchini Ofisi ya Rais (Uwekezaji) Profesa Kitila Mkumbo.
KATIKA kudhihirisha kuwa ubia kati ya kampuni ya Barrick Gold Corporation na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation unaendelea kunufaisha pande zote mbili, Migodi ya Barrick nchini imetoa gawio la shilingi bilioni 93.6 kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutunukiwa tuzo ya nafasi ya Kwanza katika makundi ambayo Serikali ina hisa chache kwa mwaka huu.
Hundi ya gawio hilo (Dummy cheque) imekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan na Meneja wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, katika hafla ya Serikali kupokea Gawio na michango kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma (Gawio Day 2025) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mwaka wa fedha wa2022/23 kampuni ya Barrick nchini pia ilishika nafasi ya kwanza kutoa gawio kwa Serikali ya kiasi cha shilingi bilioni 84 ambapo mwaka jana ilishika nafasi ya pili kwa kutoa gawio ya kiasi cha shilingi 53,482,072,393/-.
Migodi iliyopo chini ya kampuni ya Barrick na Twiga Minerals nchini ni North Mara na Bulyanhulu na Buzwagi ambao upo katika mchakato wa kufungwa.
Akiongea juu ya mafanikio haya, Meneja wa Barrick nchini, Dk. Melkiory Ngido amesema Barrick na Twiga Minerals mbali na kutoa gawio nono kwa Serikali pia imekuwa ikichangia pato la Serikali kupitia malipo ya tozo mbalimbali katika maeneo yenye shughuli za migodi yake sambamba na kuchangia kukuza uchumi wa Taifa kupitia kodi, ushuru, magawio, mishahara na malipo kwa wazabuni wa ndani.
Ameongeza kuwa, mbali na kutoa gawio la kuchangia pato la Serikali, uwekezaji wa kampuni ya Barrick nchini unaendelea kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yanayozunguka migodi yake kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zinazotolewa na migodi inayoimiliki ya North Mara na Bulyanhulu.
Kwa upande wake , Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu akiongea katika hafla hiyo amesema kampuni ya Twiga Minerals imekuwa ikifanya vizuri kwenye sekta ya uchimbaji wa madini nchini kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele.
Mchechu amesema kwamba kwa mwaka huu serikali imepata Tsh 1.28 Trilioni kama gawio , michango na makusanyo mengineo ambazo zinakwenda kuboresha sekta ya elimu , afya , miundombinu na sekta zingine mtambuka kwenye uchumi wa nchini.
Post a Comment