MGOMBEA URAIS CHAUMA NA VIPAUMBELE VYA UWAJIBIKAJI NA UADILIFU KWENYE SEKTA YA MAENDELEO

 

Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Ali Mwalimu, amewahakikishia Watanzania kuwa atakapokuwa Rais ataleta neema kupitia serikali yake yenye misingi thabiti ya uadilifu na uwajibikaji, ikilenga kuleta maendeleo ya kweli kwa kila mwananchi.


Mwalimu ametinga katika viunga vya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) majira ya saa 12 jioni tarehe 12 Agosti 2025, akiambatana na mgombea mwenza, Devota Minja, pamoja na wanachama wa chama waliosindikiza kwa bashasha, huku wakitumbuiza kwa matarumbeta na ngoma za kienyeji.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Mwalimu amesisitiza kuwa mojawapo ya nguvu kubwa ya CHAUMMA ni usafi wa rekodi na dhamiri hali inayo wawezesha kuwa wazi mbele ya Watanzania bila woga, aibu au deni lolote kwa mtu yeyote.

“Mimi ni kiongozi msafi, sina deni lolote kwa mtu, sina aibu kwa sababu ya usafi wangu wa dhamiri na matendo,mimi na mgombea mwenza ni wasafi na tunatoa fikra safi, bila mawaa yoyote ambayo yangezuia mustakabali wa taifa letu,” amesema Mwalimu, akisisitiza kuwa uwazi na uadilifu ndio msingi wa uongozi bora.

Ameongeza kuwa Kipaumbele cha chama hicho ni kuinua sauti ya wananchi na kuleta mageuzi ya kweli.

“Kampeni zetu rasmi zitazinduliwa Zanzibar, ambapo chama kitaanza kuomba ridhaa kwa Watanzania wote kutuamini ili tuwatumikie,” amesema.

Mwalimu pia aliwashukuru wananchi wa Dodoma kwa mapokezi makubwa waliompa, akisema kuwa hayo ni ishara tosha ya ushujaa wa taifa katika kusukuma mabadiliko.

Akizungumzia mabadiliko yanayokusudiwa, mgombea huyo alisema kuwa msingi wa mageuzi utaanzia katiba mpya itakayoweka wazi haki za watu wote. 

“Tukipata ridhaa tutaanzisha serikali inayolenga haki za watu na kuwahakikishia uhuru wa kweli bila hiana yoyote,” amesema.

Aidha, aliwahakikishia Watanzania kuwa rekodi safi na upya wa chama hicho ni dhamana ya uhuru na maendeleo ya taifa.

“Watanzania watarajie kuona Tanzania yenye neema na maendeleo ambayo Mungu ametupatia. Tumekulia maisha ya umaskini, lakini tunayaelewa maisha hayo na tunawapa matumaini kuondokana na hali hiyo,” ameongeza.

Mwalimu aliwataka Watanzania kujiandaa kwa mabadiliko makubwa katika uchaguzi ujao na kuahidi kupambana kwa nguvu zote ili kuleta mustakabali bora kwa taifa.

“Safari hii sio ya mtu mmoja, bali ni ya chama chote na Watanzania wote wanaotaka kuona maendeleo na mabadiliko chanya,” amesema.

Naye mgombea mwenza wa Urais kwa tiketi ya CHAUMMA, Devota Minja, aliwahimiza Watanzania kuendelea kuwaamini wanawake na kuwahakikishia kuwa hawatadhibitiwa au kudhulumiwa katika nafasi zao za uongozi.

Alisisitiza kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika kusukuma agenda za maendeleo hasa katika sekta za afya, elimu, maji, na masuala ya afya ya uzazi.

“Watanzania wanatambua uwezo wa wanawake katika nafasi za uongozi,tumeona wanawake wanaweza kusaidia kuleta mageuzi makubwa hasa katika masuala yanayogusa maisha ya kila siku,

Mimi na mgombea mwenza tutashirikiana kwa dhati kusukuma gurudumu hili kwa maendeleo ya Watanzania,” amesema Minja.




Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA