RAIS DKT. SAMIA ATUNUKIWA TUZO YA SHUKRANI KWA UONGOZI WAKE WA HURUMA NA UPENDO KWA WATU WENYE ULEMAVU

 


♻️Dar es Salaam, 11 Oktoba, 2025 

🆕Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, ameshiriki katika hafla ya kupokea Tuzo ya Shukrani iliyotolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Oysterbay, Jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDM) na kupokelewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kikwete amesema kuwa hatua hiyo ni ishara ya kutambua juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, na kwamba ni kielelezo cha uongozi wenye maono, huruma, na moyo wa upendo kwa watu wote bila ubaguzi.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni kiongozi mwenye dira na dhamira ya kweli ya kumwinua kila Mtanzania. Ameonyesha uongozi wa kipekee unaolenga usawa, haki, na ustawi wa jamii. Tuzo hii ni alama ya heshima kwa kazi kubwa na matokeo chanya anayoyaendeleza kwa vitendo,” 

"Tuzo hii pia inaonyesha shukrani za dhati kutoka kwa Watu Wenye Ulemavu nchini, wakitambua jitihada za Rais Dkt. Samia katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, hususan katika kuweka sera na mifumo jumuishi inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi", alieleza Mhe. Kikwete.

Pia aliongeza kuwa uongozi wa Rais Dkt. Samia umeweka msingi imara wa maendeleo jumuishi, unaogusa makundi yote katika jamii, na kuifanya Tanzania kuwa mfano wa nchi yenye uongozi unaojali utu na usawa.

“Tanzania imebarikiwa kuwa na kiongozi mwenye moyo wa upendo, maono makubwa, na nguvu ya kuunganisha taifa. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amethibitisha kwa vitendo kuwa uongozi ni huduma, si heshima tu,” alisisitiza Mhe. Kikwete.

Mhe. Kikwete ametoa shukrani za dhati kwa Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDM) kwa kutoa tuzo hii kutambua na kuenzi jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia katika kuboresha maisha ya Watu Wenye Ulemavu na kuendeleza maendeleo jumuishi nchini.

#RaisDktSamiaKiongoziWenyeHuruma
#UongoziUnaotumikiaWoteBilaUbaguzi
#TanzaniaInaJivuniKwaUongoziUnaojaliWote
#MaendeleoJumuishiKwaWote
#HeshimaKwaWatuWenyeUlemavu





Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA