Aliyewahikuwa Mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ambaye pia ni mwanafamilia wa karibu wa marehemu Mzee Edwin Mtei, amesema kuwa siasa za Mzee Mtei zilijengwa juu ya misingi ya maelewano, ushirikiano na kuimarisha sera, badala ya kulumbana.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili msibani nyumbani kwa marehemu Mzee Mtei, Mbowe alisema Mzee Mtei alikuwa mtu aliyependa kujenga mahusiano mema na watu wote, bila kujali tofauti za itikadi za kisiasa, ndani na nje ya chama chake.
Mbowe aliongeza kuwa tabia ya ushirikiano ya Mzee Mtei ilimfanya kuwa kiongozi wa kipekee katika historia ya siasa za upinzani nchini Tanzania.
“Alijenga mahusiano mema na watu wote na hakuwa mtu wa kuchagua marafiki. Alikuwa mtu wa kipekee sana, jambo lililomfanya kuimarisha siasa za upinzani nchini,” alisema Mbowe.
Mbowe pia alisisitiza kuwa siasa za upinzani za enzi za Mzee Mtei hazikuwa za kulumbana, bali zililenga kuunda na kuendeleza mjadala wa sera na hoja zenye kujenga.
Ameongeza kuwa mchango wake katika kuasisi na kukuza siasa za upinzani utaendelea kukumbukwa kama sehemu muhimu ya historia ya demokrasia nchini Tanzania.
إرسال تعليق