
Serikali
imetoa onyo kali dhidi ya kundi la watu wanaotumia vibaya teknolojia
kwa kukata na kusambaza vipande vya video (clips) kwenye mitandao ya
kijamii, vikiwa na lengo la kupotosha umma na kuchochea mipasuko ya
kikabila, kikanda, na kisiasa nchini.
Tahadhari
hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi,
mjini Dodoma, alipokuwa akizungumza na menejimenti ya wizara yake.
Waziri Katambi amebainisha kuwa utamaduni wa kuhariri maudhui ili kuleta
picha potofu ni "nia ovu" kisheria na ni uhujumu wa amani iliyoasisiwa
na waasisi wa Taifa hili.
Kitendo
hicho cha kukata video kinafananishwa na kuchochea balaa na kwamba
serikali haitavumilia. Aidha serikali imewaambia Watanzania kwa kauli
yake kwamba kuchochea balaa si namna bora ya kuwa binadamu na kutaka
wananchi kuona umuhimu wa kila mtumiaji wa mitandao ya kijamii
kujiridhisha na ukweli wa taarifa kabla ya kuisambaza.
Kutengeneza
video za uchochezi kunaweza kuonekana kama mchezo wa kupata "views" au
"likes," za kutosha lakini gharama yake ni kupoteza utulivu ambao
Tanzania imejivunia kwa miongo sita.
Waziri
Katambi amefafanua kuwa kuna watu wamebobea katika kukata video za
viongozi au wananchi na kuziacha bila muktadha (context), jambo
linalosababisha taharuki na kudhalilisha wahusika. Mbinu hizi zinatajwa
kutumika kama ajenda ya kusukuma mipasuko ya kijamii na kudhoofisha
umoja wa kitaifa.
"Kugawanya
viongozi kwa kutumia vipande vya video ambavyo havijazingatia usawa wa
pande zote ni kitendo cha kudhalilisha na kutweza utu. Tafsiri yake ni
kwamba aliyekata kipande hicho ana nia ovu ya kuleta taharuki," alisema
Waziri Katambi.
Ameongeza
kuwa Serikali haitasita kuwaita wahusika wa vitendo hivyo ili watoe
maelezo ya kina kuhusu dhamira yao ya kutaka kuligawa taifa. Lengo ni
kupima faida wanayoiona wao dhidi ya hasara kubwa ambayo taifa linaweza
kuipata kupitia uvunjifu wa amani.
Pamoja
na onyo hilo, Waziri Katambi amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya
Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaongozwa na falsafa ya
kutafuta suluhu (R4). Alibainisha kuwa milango iko wazi kwa majadiliano
ya kisheria na pale itakapobainika mtu yuko sahihi, haki yake itatolewa
bila upendeleo.
"Mimi
niko tayari kuzungumza na Watanzania na kuwaeleza ukweli. Sehemu
tutakayoona mtu yuko sahihi, haki yake ataipata. Huo ndiyo msingi wa
Rais Samia, mama anayetafuta suluhu na ndiyo maana ameunda hata tume
mbalimbali," alisisitiza Katambi.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohamed Mahmoud,
amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa weledi wa hali ya
juu ili kufikia matarajio ya Rais na Watanzania. Alisema kuwa maelekezo
yaliyotolewa na Waziri Katambi ndiyo yatakuwa dira ya wizara katika
kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa kwa kuzingatia haki.
إرسال تعليق