📍Manyara
MGODI wa Intracom Fertilizers Limited unaojihusisha na uchimbaji na uchakataji wa madini ya phosphate uliopo katika eneo la Vilima Vitatu Wilayani Babati Mkoani Manyara umeanza ujenzi wa mtambo mpya mkubwa wa kuchakata madini hayo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa malighafi inayotumika kutengeneza mbolea za aina mbalimbali.
Naibu Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Nestor Nibitanga, amesema kwa sasa mgodi huo una mtambo mmoja ambao haukidhi mahitaji ya soko kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa mbolea ndani na nje ya nchi.
“Mpango wetu ni kuongeza mitambo mitatu zaidi ili kufikia jumla ya mitambo minne. Hatua hii itaongeza kasi na kiwango cha uzalishaji. Kwa sasa tunazalisha kati ya tani 400 hadi 700 kwa siku, lakini mahitaji ya soko ni makubwa zaidi,” amesema Nibitanga.
Ameeleza kuwa kabla ya kuanza rasmi shughuli za uchimbaji, kampuni ililipa fidia ya Shilingi Bilioni 4.9 kwa wananchi 567 waliopisha eneo la mradi. Fidia hiyo ilihusisha nyumba, miti na makaburi yaliyohamishwa, pamoja na ujenzi wa shule mpya ya msingi kuchukua nafasi ya iliyokuwapo awali.
“Tumelipa fidia stahiki na kujenga shule mpya kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.5 ili kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na mradi hawapati athari za moja kwa moja,” amesema.
Nibitanga amesema tangu kuanza kwa mradi huo, manufaa yake yameonekana si tu kwa jamii inayouzunguka, bali pia kwa sekta ya kilimo kupitia upatikanaji wa malighafi na mbolea bora.
Ameongeza kuwa kampuni inalenga kupanua wigo wa uwekezaji kwa kuanza uzalishaji wa mbolea kamili badala ya kuishia katika malighafi pekee, hatua itakayopunguza utegemezi wa malighafi kutoka nje ya nchi.
“Dhamira yetu ni kujitegemea kwa kuzalisha mbolea kamili hapa nchini. Aidha, mbolea bora inahitaji mbegu bora, hivyo tuna mpango wa kuwekeza pia katika sekta ya uzalishaji wa mbegu,” amesema.
Amefafanua kuwa mbolea inayozalishwa na kampuni hiyo ina mchanganyiko wa asilimia 50 ya malighafi asilia na asilimia 50 ya madini, hali inayosaidia kuhifadhi rutuba ya udongo tofauti na baadhi ya mbolea za madini pekee ambazo huweza kuathiri ubora wa ardhi kwa muda mrefu.
Kwa sasa, kampuni inaendelea kufanya tafiti ili kuhakikisha kila zao na aina ya udongo vinapata mbolea inayokidhi mahitaji yake.
Mbolea ya Fomi inayozalishwa na kampuni hiyo tayari inauzwa katika masoko ya Uganda na Kenya, huku Angola na Malawi zikiwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza usambazaji.
Kwa upande wake, Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Projest Amos, amesema kiwanda cha Itracom kilichopo Nala, Dodoma kina uwezo wa kuzalisha hadi tani milioni moja za mbolea kwa mwaka, kikitumia madini ya phosphate yanayochimbwa nchini.
Amesema matumizi ya mbolea hiyo yameleta tija kwa wakulima ikilinganishwa na kipindi cha awali ambapo sehemu kubwa ya mbolea iliagizwa kutoka nje ya nchi.
“Kwa sasa wakulima wanatumia mbolea inayozalishwa hapa nchini ambapo imeonesha matokeo chanya. Mbolea ya Fomi husaidia kupunguza tindikali (pH) kwenye udongo na kuboresha uchukuaji wa virutubisho, hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini,” amesema Amos.





Post a Comment