WAFANYABIASHARA - MAGOMENI KUENDELEA KUNUFAIKA NA MIKOPO INAYOTOLEWA NA SERIKALI

 



Na Abdala Sifi WMJJWM-Dar Es Salaam

Wafanyabiashara ndogondogo katika soko la Magomeni mkoani Dar es Salaam, wameeleza kunufaika na Mikopo inayotolewa na Serikali kwa kusimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamiii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum kupitia Benki ya NMB.

Wameeleza hayo tarehe 26 Februari 2025 mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.John Jingu alipotembelea soko hilo kwa lengo la kuzungumza nao na kujionea namna walivyonufaika na mikopo inayotolewa na Serikali kupitia benki ya NMB ili kuwawezesha kuimarisha na kukuza biashara zao.

Katika ziara hiyo, Dkt. Jingu alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali na kusikiliza mafanikio ya wafanyabiashara hao. Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa mikopo kwa makundi maalum, hususan wanawake na vijana, ili kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa kipato cha chini.

"Nimezunguka na kuwasikiliza wafanyabiashara ndogondogo hapa sokoni, wameeleza kunufaika na Mikopo inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Nimefurahi kwamba mnaendelea kufaidika na Mikopo hii, nia ya Serikali ni kuhakikisha mnakuza mitaji pamoja na biashara zenu".amesema Dkt.Jingu.

Akizungumza katika soko hilo, Sofia Mohamed mfanyabiashara ndogondogo, amesema mkopo alioupata umemsaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha biashara yake huku akifafanua kuwa ameongeza mtaji, kupanua wigo wa bidhaa anazouza na hivyo kuongeza kipato chake cha kila siku.

“Mkopo huu umenisaidia sana. nimeweza kuongeza bidhaa na wateja wangu wameongezeka,” amesema Sofia

Kwa upande wake, George Mbena, ambaye naye anafanyabiashara katika soko hilo, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha na kuendeleza utoaji wa mikopo hiyo huku akisema mikopo imewasaidia wafanyabiashara wengi kuimarisha biashara zao na kukuza mitaji yao. George ameiomba Serikali kuongeza kiwango cha mikopo ili kuwawezesha kupiga hatua zaidi kibiashara.

Ziara hiyo imeonesha dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi, kusikiliza maoni yao na kuhakikisha kuwa mikakati ya kiuchumi inaleta matokeo chanya.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA