Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Septemba 4, 2026.
Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Agosti 25, 2026, Nchimbi amesema amefanya uamuzi huo kwa mujibu wa Ibara ya 50(2)(c), ikisomwa pamoja na Ibara ya 149(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nchimbi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kumsaidia katika uongozi wa Serikali.
Amesema tangu Agosti 27, 2025, alipomwahidi Rais Samia kuwa atamsaidia kwa uwezo wake wote na kwa uaminifu, amekuwa akitekeleza ahadi hiyo.
Aidha, amemshukuru Rais Samia pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa imani waliyomwonyesha, akisema ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Watanzania wote kwa ushirikiano waliompa wakati wote aliokuwa katika utumishi wa umma.
Taarifa hiyo imetolewa na Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 25 Agosti 2026.


Post a Comment