
Na WMA - DODOMA.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amefurahishwa na uelewa mkubwa ulioonyeshwa na wanafunzi waliopata elimu ya vipimo katika banda la Wakala wa Vipimo - (WMA), kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane.
Akizungumza leo Agosti 6, 2026 baada ya kuzungumza na wanafunzi hao aliowakuta katika Banda la WMA, Viwanja vya Dkt. John Malecela Nzuguni, Dodoma, Naibu Waziri ambaye pia alikuwa katika ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali ya Maonesho, alisema ni hatua nzuri kwa WMA kuanza kuwafundisha watoto umuhimu wa vipimo sahihi wakiwa wadogo.
“Nimefurahishwa sana. Watoto hawa wameelewa kuwa kipimo sahihi ni haki ya kila mtu. Hawa ndio Maafisa Vipimo wa kesho,” alisema.
Awali, Naibu Waziri Chande alipowakuta wanafunzi hao bandani aliwauliza maswali mbalimbali kuhusu vipimo na waliweza kujibu kwa ufasaha.
Wanafunzi hao wa Shule ya Msingi Blessed Mabuba iliyopo jijini Dodoma, ambao waliongozana na mwalimu wao Irene Ketta, ambaye pia alipongeza WMA kwa kujielekeza katika utoaji elimu ya vipimo mashuleni hatua ambayo alisema imewawesha wanafunzi kueleza tofauti ya kipimo sahihi na kisicho sahihi, umuhimu wa kusoma lebo na jinsi ya kutumia mizani.
“Niwape pongezi WMA. Kama tutaendelea kuwapa elimu hii watoto wetu, tunajenga Taifa la wafanyabiashara waaminifu na walaji wenye ufahamu. Huu ndio msingi wa uchumi imara,” alisema Mwalimu Ketta.
WMA imeahidi kuhakikisha elimu ya vipimo inaenea kwa jamii nzima kupitia utoaji elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi.



Post a Comment