ASILIMIA KUBWA YA WANAWAKE WANASHIRIKI KILIMO, UFUGAJI - WAZIRI MKUU


   
*Asema uwekezaji ni lazima ili Afya Moja ifanikiwe katika ngazi ya jamii 

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema takribani theluthi mbili ya wanawake walioajiriwa katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwemo, hufanya kazi kwenye mifumo ya chakula na kilimo.

“FAO inakadiria kuwa wanawake wanaunda zaidi ya asilimia 42 ya nguvu kazi katika mifumo ya chakula na kilimo duniani. Takwimu hizi zinaonyesha kwamba wanawake hawako pembezoni mwa mifumo ya chakula na kilimo; bali wako katika kiini cha mifumo hiyo,” amesema.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akishiriki jopo la viongozi wa juu lililojadili Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima – Mtazamo wa Afya Moja, lililofanyika katika Kituo cha Sheikh Zayed, Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia. 

Waziri Mkuu ambaye anashikiri Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema yeye mwenyewe anatoka katika jamii ambako sehemu kubwa ya shughuli za uzalishaji, hasa za kilimo na ufugaji, hufanywa na wanawake.

“Katika jamii zetu nyingi, shughuli hizi mbili za kiuchumi zinaongozwa na wanawake, lakini mchango wao bado unakabiliwa na vikwazo, ikiwemo ukosefu wa fursa sawa ya kupata ardhi, fedha, teknolojia, huduma za ugani, masoko na kushiriki katika kufanya maamuzi,” alisema wakati akitoa mada yake kwenye jopo hilo llililowashirikisha mawaziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi kutoka Ufaransa na Ireland na kuongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Godfrey Magwenzi.

Akifafanua zaidi, Dkt. Mwigulu alisema: “FAO inakadiria kwamba hata pale wanawake wanaposimamia mashamba yenye ukubwa sawa na yale yanayosimamiwa na wanaume, tofauti ya uzalishaji kwa kila eneo la ardhi kati ya wanawake na wanaume ni takribani asilimia 24. Wanawake wanaofanya kazi katika ajira zenye malipo ndani ya mifumo ya chakula na kilimo hupata, kwa wastani, asilimia 78 ya kipato kinachopatikana kwa kila dola anayopata mwanaume.”

“Hizi si takwimu tu zinazoonyesha ukosefu wa usawa; zinawakilisha pia uzalishaji unaopotea, kipato kinachopotea na fursa zinazopotea za kujenga mifumo imara na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za chakula. Na hapo ndipo dhana ya Afya Moja inapopata umuhimu mkubwa,” alisisitiza.

Alisema mwanamke mkulima haoni afya ya binadamu, ya wanyama, ya mimea na ya mazingira kama sekta zinazojitegemea kwa kuwa analima chakula kwa ajili ya familia na jamii, anafuga mifugo, anasimamia maji na ardhi, anahifadhi na kusindika chakula, anafanya maamuzi kuhusu afya ya wanyama na lishe ya familia, na anakabiliana na ukame, mafuriko, wadudu na magonjwa.

“Kwa hiyo, maamuzi yake yanaweza kuathiri lishe, usalama wa chakula, kinga dhidi ya magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, matumizi sahihi ya dawa za kuua vimelea, bioanuwai na uendelevu wa mazingira.”

“Kumwezesha mwanamke ni kuwekeza si katika kilimo pekee, bali pia katika Afya Moja. Ikiwa tunataka Afya Moja ifanikiwe katika ngazi ya jamii, ni lazima tuwekeze kwa wanawake ambao tayari wanaitekeleza katika maisha yao ya kila siku,” alisisitiza.

Akishiriki mjadala huo, Waziri wa Kilimo na Chakula wa Ufaransa, Bi. Annie Genevard alisema licha ya kuwa Ufaransa ni nchi inayohamasisha usawa kati ya wanaume na wanawake, bado kuna mazingira ambayo wanawake wanahisi kutoonekana.

“Robo ya mameneja wa mashamba nchini Ufaransa ni wanawake. Si jambo la kushangaza kusikia mwakilishi wa mauzo (sales representative) anapofika shambani na kumuuliza mwanamke anayemkuta: “Ningependa kumuona bosi wa hili shamba.” Nao hujibu: “Mimi ndiye bosi.”  

Amekiri kuwa, bado kuna safari ndefu ya kufikia usawa na kwamba hawawezi kujenga mifumo ya kilimo na chakula yenye ustahimilivu zaidi bila kuchukua hatua kwa wakati mmoja kupunguza ukosefu huo wa usawa.

Alisema alipoteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, aliamua kuanzisha mpango wa kuwainua wanawake kupitia mafunzo na kuongeza muonekano wao wa umiliki kwenye jamii yao. Lengo lake ni kuwasaidia zaidi wanawake wakulima katika maisha yao ya kila siku ili wapate taarifa bora kuhusu haki zao, hususan kuhusu uzazi, kuboresha huduma za kuchukua nafasi ya mkulima na kuboresha zaidi zana za kilimo ili ziendane na mahitaji yao.

“Na niseme wazi hapa kuwa hatuko katika hatua ya kutoa ahadi pekee; tayari tumeanza kuchukua hatua. Tumeanza kuwatambua wanawake katika kilimo na pia kuwawezesha kutambuliwa kama wakulima kamili. Zaidi ya hayo, tumehakikisha mpango huu unaweza kupimwa na kufuatiliwa kwa muda.  Kila hatua ina viashiria vya ufuatiliaji na matokeo.”

Naye, Waziri wa Kilimo, Chakula na Masuala ya Uvuvi wa Ireland, Martin Heydon aliwaeleza washiriki wa jopo hili kwamba kabla hajawa Waziri wa Kilimo, alikuwa mkulima katika shamba alilorithi kutoka kwa mama yake.

“Mimi na mke wangu bado tunaendesha shughuli za kilimo pamoja na watoto wetu wanne katika shamba letu. Shamba hilo nilirithi kutoka kwa mama yangu, kwa sababu baba yangu alifariki nilipokuwa na umri wa miaka minane tu,” alisema.
“Mwaka 1986 wakati baba anafariki, mama yangu alikuwa na miaka 43. Alikuwa mama na baba yetu kwa wakati mmoja. Wakati mwingine alikuwa mwalimu wetu, muuguzi wetu, lakini daima alikuwa mkulima. Alisisitiza kuendelea na shughuli za kilimo wakati akitulea. Alitaka kutujengea upendo, shauku na maarifa kuhusu uzalishaji wa chakula, kutunza wanyama, kutunza ardhi na mambo mengine yanayohusiana na kilimo.” 

Alisema kuwa, kwa uzoefu wa Ireland, wanawake wakulima, madaktari wa mifugo wanawake, wanasayansi wanawake wa kilimo na watafiti wanawake wa mimea wako katika kiini cha maeneo yote hayo lakini mara nyingi mchango wao hautambuliwi kwa kiwango kinachostahili. 

“Wanawake bado ndiyo walezi wakuu katika kaya nyingi za vijijini nchini Ireland, wakishiriki katika kupanga lishe ya familia, usalama wa chakula nyumbani na kubeba mzigo wa kiafya pale kipato cha shamba kinapokuwa hakina uhakika au majukumu yanapokutana na kazi za nje ya shamba. Mkakati wowote makini wa Afya Moja lazima uzingatie kazi hii isiyolipwa na ambayo kwa kiasi kikubwa haionekani kama sehemu ya mfumo huo,” alisema.

Alisema kizazi kipya nchini humo kinahusiana na maeneo yote hayo lakini kuna wakulima wachache sana ambao wana umri chini ya miaka 35. “Urithi wa mashamba nchini Ireland kwa muda mrefu umekuwa ukifuata utamaduni wa kumrithisha mwanaume. Tume yetu huru kuhusu kizazi kipya katika kilimo iliweka wazi kwamba kusaidia urithi wa mashamba na kuboresha usawa wa kijinsia ni jukumu moja, si mambo mawili tofauti. Binti yangu mwenye umri wa miaka mitano, ana nafasi sawa kabisa ya kurithi shamba letu kama ndugu zake watatu wa kiume,” alisisitiza.

Waziri huyo alisema anaamini kwamba ili kuwa na uendelevu wa kweli katika nyanja za kiuchumi, kimazingira na kijamii, ni lazima kuhakikisha wanawake wanakuwa na nafasi sawa na wanaume katika mifumo ya chakula na kilimo. 

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amefuatana na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na watendaji wengine wa Serikali














Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA