Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeendelea kuimarisha usimamizi wa usalama wa mionzi nchini kupitia operesheni ya ukaguzi wa vituo vinavyotumia vifaa na vyanzo vya mionzi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kuhakikisha matumizi ya mionzi yanafanyika kwa usalama.
Operesheni hiyo inayotekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya mwaka 2003, inalenga kuhakikisha vituo vinavyotoa huduma zinazohusisha matumizi ya mionzi vinakuwa na leseni halali, wataalamu wenye sifa zinazotakiwa pamoja na vifaa vilivyo katika hali nzuri na vinavyokidhi viwango vya usalama.
Katika Mkoa wa Pwani, TAEC ilifanya ukaguzi kuanzia Septemba 2 hadi 16, 2026, ambapo timu ya wataalamu wa Tume ilitembea umbali wa takribani kilomita 1,450 katika maeneo ya Kibaha, Bagamoyo, Kisarawe, Kibiti, Rufiji, Mkuranga na Mafia.
Jumla ya vituo 35 vilikaguliwa katika mkoa huo, vikiwemo hospitali, vituo vya afya na kliniki, pamoja na maeneo mengine yanayotumia vifaa au vyanzo vya mionzi, ikiwemo viwanda na maeneo yenye mifumo ya ukaguzi wa mizigo.
Matokeo ya ukaguzi huo yanaonesha kuwa vituo 19 kati ya 35 vilivyokaguliwa vilikidhi mahitaji muhimu ya usalama wa mionzi na kuwa na leseni halali. Vituo 16 vilibainika kuwa na mapungufu mbalimbali yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ili kukidhi matakwa ya sheria na viwango vya usalama.
Miongoni mwa mapungufu yaliyobainika ni baadhi ya vituo kutoa huduma bila kuwa na leseni halali, kutokidhi baadhi ya masharti ya usalama, kuwa na mashine zinazohitaji matengenezo pamoja na kukosekana kwa wataalamu wenye sifa zinazotakiwa. Baadhi ya vituo pia havikuwa vikitoa huduma zinazohusisha matumizi ya mionzi wakati ukaguzi ulipofanyika.
Akizungumzia ukaguzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TAEC, Peter Ngamilo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya majukumu ya Tume ya kuhakikisha matumizi ya mionzi nchini yanafanyika kwa usalama kwa wagonjwa, watumishi na wananchi kwa ujumla.
“Tunafanya ukaguzi huu kuhakikisha huduma zinazohusisha matumizi ya mionzi zinatolewa kwa kuzingatia usalama wa mgonjwa, mtoa huduma na wananchi. Katika Mkoa wa Pwani, vituo 19 kati ya 35 vilivyokaguliwa vimekidhi mahitaji muhimu, huku vituo 16 vikibainika kuwa na mapungufu yanayopaswa kurekebishwa,” amesema Ngamilo.
Amesema TAEC itaendelea kuvifuatilia vituo vilivyobainika kuwa na mapungufu na kutoa maelekezo ya kitaalamu ili viweze kurekebisha kasoro hizo na kukidhi matakwa ya sheria.
Ngamilo ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa ukaguzi katika Mkoa wa Pwani, TAEC imeendelea na operesheni hiyo katika maeneo mengine nchini, ambapo vituo 32 vimekaguliwa katika Mkoa wa Lindi na vituo 40 Zanzibar. Hivyo, jumla ya vituo 107 vimekaguliwa katika Pwani, Lindi na Zanzibar.
Amesema ukaguzi pia umefanyika katika Mkoa wa Njombe na taarifa zake zinaendelea kuchakatwa, huku operesheni hiyo ikiendelea hivi sasa katika Mkoa wa Morogoro.
Amesisitiza kuwa dhamira ya TAEC katika ukaguzi huo ni kuhakikisha sheria na taratibu za usalama wa mionzi zinazingatiwa, sambamba na kutoa elimu na maelekezo ya kitaalamu kwa wamiliki na waendeshaji wa vituo vinavyotumia vifaa na vyanzo vya mionzi.
“Tunatoa wito kwa wamiliki na waendeshaji wa vituo vinavyotumia vifaa au vyanzo vya mionzi kuhakikisha wana leseni halali, vifaa vyao vinakidhi viwango na wana wataalamu wenye sifa zinazotakiwa. TAEC itaendelea kufanya ukaguzi na kutoa elimu ili kuhakikisha matumizi ya mionzi nchini yanafanyika kwa usalama,” amesema Ngamilo.
Ameongeza kuwa usimamizi madhubuti wa matumizi ya mionzi ni muhimu katika kulinda afya za wagonjwa, watumishi wanaofanya kazi katika mazingira yenye mionzi, wananchi pamoja na mazingira.











Post a Comment